Bure Ukusanyaji wa KAWAKIA

Vifungu vyote viliunda au kuwasilishwa wakati wa miaka ishirini ya kwanza ya mradi huo, kutoka 1995 hadi 2015.

Lumwe Ng’ombe, Yakobo

1888-1976
Waprotestanti
Tanzania

image Yakobo Lumwe, ambaye pia aliitwa Yakobo Ng’ombe, alikuwa ni Mchungaji wa kwanza mwenyeji wa kanisa la kiprotestanti pwani ya kaskazini mwa Tanganyika. Alitumika ndani na katika mzunguko wa maeneo ya Tanga mjini, sehemu ambayo sasa ni ya Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri katika Tanzania. [1] Maisha yake na kazi ni mfano wa kusifu jinsi gani wakristo wananchi walivyojishughulisha katika kueneza Injili na kujenga kanisa pamoja na wageni wamissionari.

Yakobo Ng’ombe alizaliwa miaka ya 1880, wakati ule ilikuwa ni wakati wa “Vita vya Kilindi,” ilikuwa ni ugomvi kati ya machifu wa Wakilindi wa Milima ya Usambara na Wabondei. Katika wasifu wake mfupi [2], aliandika kwamba “Wazee wanaojua vita hivyo wanasema vilikuwa mwaka wa 1888.” [3] Jina la mahali alipozaliwa ilikuwa ni Mgambo [4], ni kijiji kidogo upande wa kaskazini magharibi mwa Tanga mjini, katika sehemu ya nchi ya Wabondei, kwa watu wa upande wa Baba yake. Baba yake Lumwe, [5] Mwislamu mtiifu, aliyekuwa na wananwake wengi, [6] alifanya kazi kama mfua chuma na baadaye kama mfanyabiashara; Mama yake Kurawira [7] alikuwa Mdigo [8], watu ambao wanaishi kaskazini mwa Tanga mjini. Yakobo aliitwa Lumwe, kama Baba yake. Jina lake lingine aliitwa Ng’ombe [9], jina hili lilitoka kwa Babu yake, ambaye aliishi pamoja naye kwa muda wakati wa utoto wake.

Mara baada ya kufariki baba yake, mama yake Kurawira aliacha ndugu wa mume wake, na kuhama pamoja na watoto wake kwenda kwenye kijiji cha Mwenzage karibu na Tanga mjini. Yakobo kwa muda aliishi pamoja na shangazi yake na akajiunga na shule ya karibu ya missioni katika Shwari, [10] shule ambayo ilianzishwa na August Krämer [11], mmissionari wa kwanza wa Evangelical Mission Society for German East Africa (EMS) [12] katika Pwani ya Kaskazini mwa Tanganyika ambapo wakati ule iliitwa Deutsches Schutzgebiet (“German Protectorate”) [13].

Baada ya muda fulani wanafunzi walikwenda shuleni pale Mbuyukenda, makao makuu ya missioni Tanga mjini. [14] Pale Yakobo alijiunga kwenye kozi, kwa ajili ya kujiandaa kwa ubatizo, hasa kwa kushauriwa na marafiki zake.Wakati wa mafundisho alianza kuelewa tabia ya Mungu, “Kwamba ni Baba, zaidi tukiomba sala ya Bwana. Nikafurahi, nikatumaini kama nimepata Baba, kama wa duniani sina, huyu wa mbinguni anatosha.” [15] Alikuwa ni mwanafunzi mwenye hamu sana, hivyo Mchungaji Martin Ostwald [16] mmsionari aliyembatiza mwaka mmoja baadaye, aliandika katika mwaka wa 1898, “Inaelekea anafahamu Biblia na Katekisimo, pia hesabu, kusoma na kuandika vizuri zaidi kuliko wenzake wa rika lake wa Ujerumani.” [17]

Mnamo Januari 29, 1899 [18] Yakobo alibatizwa katika kanisa la Mbuyukenda karibu na Bahari ya Hindi pamoja na vijana wa kiume watano. Miongoni mwa hao alikuwa Paulo Pera, ambaye baadaye ndiye aliyezindua shule ya kwanza ya kiprotestanti katika eneo la Gombero katika nchi ya Wadigo. [19] Kwa muda fulani Yakobo alifanya kazi ya ndani kwa mmissionari Ostwald akisaidia kazi kama mpishi. Katika jamaa yake alijisikia vizuri, na wakati fulani ilikuwa hatari alipougua, aliuguzwa na Mama Ostwald. “Hapa nimeona upendo wa Yesu,” hilo alilikumbuka baadaye. [20]

Miaka iliyofuata alipata uzoefu katika kazi nyingine. Kulipotokea uhitaji wa lazima kwa ajili ya mwalimu kwa shule ya missioni hapo Mbuyukenda. Ernst Liebau, mmissionari aliyemfuata Martin Ostwald, [21] alimwomba Yakobo Ng’ombe afundishe. Yakobo alikubali na wakati huo huo alipata mbinu za masomo katika shule ya serikali mjini na baadaye aliendelea kupata masomo halisi kwa kupata elimu ya ziada katika shule ya serlikali Kisarawe karibu na Dar-es-Salaam. Baada ya muda mfupi kijana mwenye kipawa aliongoza pia sala pamoja na ibada Tanga mjini na katika eneo la Wadigo.

Januari 1906 akamwoa Kristine Fatuma, [22] ambaye alibatizwa katika mwezi wa Oktoba 1900. Wanandoa hawa walikuwa na watoto watatu: [23] Yohana Petro (aliyezaliwa 1906), Chamungu (aliyezaliwa 1917) na Mzaliwa Wanuru (aliyezaliwa 1927). Mke wake alimsaidia katika huduma kwenye Kanisa na pia alitumika kama mshauri mzuri kwake. Hili lilikuwa ni muhimu sana hasa wakati wa shida, kwa mfano alipokuwa akipigana na swali la kuwa Mkristo wa kawaida kuishi kama mkulima badala ya kufanya kazi ya missioni. Mmissionari Siegfried Delius [24] aliyekuwa kiongozi wa missioni Tanga kutoka mwaka 1904 hadi 1916, alimshauri Yakobo Lumwe aendelee katika njia aliyochagua.

Mwaka wa 1916 wamissionari Wajerumani ilibidi waondoke Tanga kwa vile nchi ilikuwa imechukuliwa na wanajeshi wa Kiingereza wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia. Hivyo wajibu wa kutunza sharika Tanga mjini na kwenye maeneo yake walipelekwa kwa Yakobo Ng’ombe. Hapa pia akawa kiongozi mwangalizi wa mashule Manyinyi, Udigo, iliyoanzishwa na mwenyeji mwalimu Paulo Pera. Kwa mara ya kwanza katika historia yake, kanisa changa katika pwani kaskazini ya Tanganyika ilisimama kwa miguu yake mwenyewe, bila msaada toka kwa wamissionari.

Yakobo Lumwe alichukua nafasi ya kazi yake mpya kwa makini na katika mwezi Julai, 1916 alipanga mkutano wa walimu wa Udigo katika kijiji cha Vunde. [25] Mwaka huohuo wakati wa majira ya kiangazi walipatana taratibu za kufuata wakati ujao: “1. Tusiache kusali kila siku na jumapili. 2. Tuwafundishe watoto wetu kusoma na neno la Mungu. 3. Tufanye bidii kulima mashamba yetu. 4. Tuamkiane tujuane shida, tusaidiane na kuonyana.” [26] Mmissionari Siegfrid Delius aliandika baada ya kukutana na sharika kwa mara ya mwisho,”Nilipata maoni ya kwamba Yakobo amekamilisha wajibu wake kwa bidii na shauku na alikuwa na imani kubwa kwa wakristo na kipekee pia kwa wafanyakazi wenzake.” [27]

Ilikuwa mwanzo wa matatizo katika vipindi fulani kwa mwalimu kijana kwa sababu usimamizi wa Waingereza wa Tanganyika Territory waliweka vipingamizi vingi kwenye sharika ambazo zilianzishwa na missioni ya Kijerumani. Katika hali hii ya kisiasa baadhi ya Waislamu walifanya maisha kuwa magumu kwa wakristo. [28]

Mmissionari Franz Gleiss [29] aliyeishi karibu Milimani Usambara, alimuunga mkono Yakobo Ng’ombe iwezekanavyo kwa umbali. Wakati wamissionari Wajerumani wa mwisho waliobaki milimani walipokea amri kuondoka nchini, waalimu wa kienyeji saba waliwekwa wakfu kuwa wachungaji. Miongoni mwao alikuwa Yakobo Lumwe, ambaye alikuwa wa kwanza mchungaji mwenyeji wa kanisa la kiprotestanti katika pwani kaskazini mwa Tanganyika. Katika kitabu chake binafsi aliandika juu ya ibada hiyo ya kuwekwa wakfu, iliyofanyika milimani Februari 22, 1920: “Ilikuwa ni siku kubwa ya pekee. Maelfu ya wakristo walikuja Vuga kushuhudia tukio hilo. Ilikuwa kama sherehe ya ndoa. Mara baada ya kuwekwa wakfu tulianza utumishi wetu kwa kushrehekea ushirika wa chakula cha Bwana.” [30] Kwa miaka iliyofuata uongozi wa sharika zote ulikuwa mikononi mwa wachungaji wenyeji. Sharika zilipokea msaada wa fedha mdogo sana kutoka missioni Ujerumani na ilibidi walipe mishahara kwa waalimu na kwa wachungaji wao kwa njia zao wenyewe.

Yakobo Ng’ombe alihusiana na Franz Gleiss na wamissionari wengine wa Ujerumani, kuwataarifu hali halisi ya maisha na kazi ya wakrito katika pwani. [31] Jambo la pekee ilikuwa ni kuhusu kazi ya ujenzi wa kanisa ndogo la Tanga katika mwaka 1922. [32] Jengo hilo jipya lilikuwa ni muhimu, kwa sababu usharika ulizuiliwa kufanya mikutano katika jengo la kanisa lililojengwa 1889 ambalo lilikuwa limepata uharibufu mkubwa kutokana na vita na tetemeko la ardhi.

Wakati utawala wa Kiingereza ulipowaruhusu wamisionari wa kwanza kurudi nchini Tanganyika Territory katika mwaka wa 1925, walianza kufanya kazi katika Milima ya Usambara, sio Tanga. [33] Kwa hiyo Yakobo Lumwe alibaki peke yake mchungaji kaskazini pwani mkoani, na Franz Gleiss aliendelea kumuunga mkono kutoka Usambara.

Haikuwa kwamba hadi mwaka wa 1933, kuwa mmissionari mwingine mjerumani alirudi kuishi Tanga tena na kufanya kazi pamoja na Yakobo Ng’ombe. Huyu mchungaji, Ernst Dammann, [34] baadaye alifahamika vizuri kama mtaalamu katika Lugha za Kiafrika. Alihifadhi baadhi ya maandishi yaliyoandikwa kwa mkono ya Yakobo Ng’ombe na pia kuchapisha “Safari ya Bukoba” [35] kitabu cha Yakobo Lumwe cha kumbukumbu, safari ya Buhaya, Magharibi Tanganyika, katika mwaka wa 1930. Alichaguliwa pia kumsindikiza Kurt Ronicke wa Bethel– Mission aliyekuwa mwangalizi mkuu wakati ule, kwa safari ya kutembelea. Hii ilikuwa ishara ya kuwa alifikiriwa kuwa mtu mwenye umuhimu.

Kutoka Septemba 1939 na kuendelea, tena madaraka ya sharika za Tanga na maeneo yaliyozunguka ikawa chini ya Yakobo Ng’ombe [36], kwa sababu mfuasi wa Dammann mmissionari Karl Wohlrab [37] aliwekwa kizuizini kwa ajili ya kuzuka kwa Vita ya Pili ya Dunia. Wakati huo huo mwalimu wa zamani kwenye shule ya kanisa ya Kilulu, kaskazini mwa Tanga, Imanuel Ng’anzi Vesso [38], aliwekwa wakfu na alifanya kazi pamoja na Yakobo Ng’ombe. Baada ya muda mfupi mchungaji kijana Mathayo Jengo [39], ambaye kwanza alikuwa mwinjilisti, alifanya kazi nao.

Kazi ya Yakobo Lumwe pwani ya kaskazini mwa Tanganyika Territory iliingiliwa kuanzia 1943 kwa muda wa miaka mitano Dar-es-Salaam. [40] Aliitwa kusaidia kanisa pale lililokuwa katika hali ya matatizo, baada ya mchungaji mwingine kusimamishwa kazi. Kipindi hicho Imanuel N. Vesso alikuwa kiongozi wa Usharika wa Tanga mjini. S. Hjalmar Swanson, katibu kiongozi wa Shirika la Kurugenzi ya Missioni ya Kigeni la Sinodi ya Augustana, alitembelea Dar-es-Salaam 1945 na alivutiwa sana na Yakobo, “Usharika ulitumikiwa na mheshimiwa Mwafrika kutoka Tanga kwenye maeneo ya kaskazini, Mchungaji Jakobo, ambaye Mjerumani mmoja aliandika juu yake … ‘Huyu Yakobo peke yake ni mwenye thamani kwa safari ya Afrika.’” [41] Yakobo Ng’ombe hakuangalia tu usharika wake katika mji lakini pia aliitwa kuhubiri katika sehemu zingine kama vile Bagamoyo. Kwa nyongeza alikuwa ni mwenye kazi nyingi akifundisha Dini ya Kikristo kwenye mashule ya serikali ya kienyeji. Mwishoni mwa kukaa kwake pia kulikuwa na matatizo pamoja na mchungaji kutoka Milima ya Usambara aliyefanya kazi pale Dar-es-Salaam. Baada ya muda Yakobo akaomba ahamishiwe kurudishwa Tanga mahali alipotumia muda wake akiwa kazini kama mchungaji hadi mwaka 1957, mwaka aliostaafu. [42]

Mchango wake

Katikati ya theologia ya Yakobo Lumwe, siku zote alikuwa ni Yesu Kristo, ambaye anatoa msamaha wa dhambi na maisha mapya. [43] Alijaribu kuwa na msimamo huo huo kama Yesu (Wafilipi 2:5). Kusudi lake lilikuwa ni kufanya kazi katika Ufalme wake Mungu, bali kamwe hakuwa na hamu kushika ofisi kama ile ya mchungaji. Hivyo baada ya kipindi fulani cha wasiwasi alikubali kuwekwa wakfu.

Ingawa hakuwa amepata elimu ya kitaaluma wale wachungaji wenyeji wa vizazi vilivyofuatavyo walifurahia, yeye alipata mazoezi ya Theologia kutoka wamissionari na kuwa na utaalamu wa elimu ya Biblia. Alizungumza Kiswahili vizuri ya kwamba Karl Roehl, ambaye alitafsiri Biblia katika lugha hii [44], alimtumia mswadajaribio ili aweze kusahihisha.

Wajibu wa Yakobo Ng’ombe kama mchungaji, ilikuwa ni muhimu kuhubiri Injili na kuwapata wengine kuwaleta kwa Yesu Kristo. Ushauri katika usharika, hospitali, na magereza pia kufundisha elimu ya kikristo na kozi za kubatiza ilikuwa ni wajibu wake pia. Katika kufanya haya siku zote aliheshimu utamaduni wa watu alioishi na kufanya kazi nao. Mchungaji Godfrey Hermann alisema juu yake, “Atakumbukwa kwa uvumilivu, upendo na diplomasia yake. [45]

Jambo kubwa juu ya mchango wake aliotoa, ilikuwa ni kuunganisha sharika pamoja katika wakati wa matatizo, wakati wageni wamissionari walipokuwa hawapo wakati wa vita. Yakobo Lumwe anaweza kuhesabika kuwa ni miongoni mwa wale wenye bidii, waliojitoa katika hatua za mwanzo wa kanisa changa ambalo linakua katika uhuru. [46]

Yakobo Lumwe alikufa, akiwa anakaa na mtoto wake wa kiume Chamungu huko Dar-es-Salaam Juni 27, 1976. [47] Alikuwa mchungaji mprotestanti wa kwanza wa pwani ya kaskazini mwa Tanganyika, ambayo leo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku mbili baadaye alizikwa huko Tanga, mahali pale, alipofanya kazi karibu maisha yake yote. Mwisho wa maelezo yake ya miaka 1914 - 1923 inatosha kufupisha maisha yake yote: “si mimi, ila neema ya Mungu pamoja nami.” [48]

Christian Pohl


Notes:

 1. www.elct-ned.org

 2. Autobiography I, hadi mwaka wa 1914: Berlin State Library - Prussian Cultural Heritage, Oriental Department, Hs. or. 9970 (Kiswahili, kuandikwa kwa mkono). Autobiography II, 1914-1923: Archives and Museum Foundation Wuppertal, M 656, 385ff (Kiswahili, kunadikwa kwa typewriter).

 3. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 1a.

 4. Godfrey P. Hermann, “The Work of Yakobo L. Ngo’mbe, Pioneer Pastor of the Tanganyika Coast 1920 - 1957” (thesis, Makumira University College, 1986), 4.

 5. Tanga Lutheran Parish, Family Book (Tanga, 1897 - 1953), 4.

 6. Hermann, 4.

 7. Family Book, 4.

 8. “The Digo are a Bantu tribe occupying the coastal plain between Mombasa, Kenya, and Tanga, Tanzania.” Erling A. Lundeby, “The Digo of the South Kenyan Coast: Description and Annotated Bibliography” (Thesis, Fuller Theological Seminary, 1993), 1.

 9. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 1a.

 10. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 1b.

 11. August Krämer aliishi na kufanya kazi huko Tanga kuanzia 1890 hadi 1895: Katika mwaka wa 1896 alifariki wakati alipoishi kwenye kituo cha afya huko Misri.
 12. “Shirika la Kimissioni la Kiprotestanti kwa Afrika Mashariki Kijerumani” (EMDOA) wakati fulani limefahamika kuwa Berlin III; mnamo mwaka wa 1920 na kupewa jina la Bethel-Mission.

 13. Neno “Schutzgebiet” ni usafidi wa Kikoloni, kwa kawaida imetafsiriwa kuwa ni maeneo yaliotengwa au yaliolindwa.

 14. Wahaki T. Vesso, Digoland. Andiko la Kumbukumbu Miaka 100 (1890 - 1980). Jimbo la Pwani, 2nd ed. (Tanga: unpublished, 199x), 2.

 15. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 2a.

 16. Martin Ostwald, aliyempokea August Krämer aliishi na kufanya kazi Tanga kuanzia mwaka wa 1896 hadi 1902.

 17. Siegfried Delius, Gute Saat auf hartem Boden, 2nd ed. (Bethel near Bielefeld: Publishing House of the Evangelical Mission Society for German East Africa, 1911), 68. Kwa Kijerumani: “Er weiß in der Bibel und im Katechismus vielleicht besser Bescheid, ebenso im Rechnen, Lesen und Schreiben, als wohl mancher gleichaltrige Bursche in Deutschland.”

 18. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 2b, and Family Book, 4.

 19. Tazama DACB wasifu wa Paulo Pera (Mprotestanti Tanganyika).

 20. Autobiograpy I, Hs. or. 9970, 2b.

 21. Ernst Liebau, mfuasi wake Martin Ostwald, aliishi na kufanya kazi Tanga kuanzia mwaka wa 1902 hadi 1903.
 22. Family Book, 4; Autobiography I, Hs. or. 9970, 3b.

 23. Family Book, 4.

 24. Siegfried Delius, mfuasi wake Enrst Liebau, aliishi na kufanya kazi Tanga kuanzia mwaka wa 1904 hadi 1916; mnamo katika 1917 aliwekwa kizuizini na jeshi la Kingereza katika Tanga na kuhamishiwa kwenye kambi huko Misri.

 25. Ernst Dammann, barua (Pinneberg: isiyochapishwa, 14.08.1985), 2.

 26. Autobiograpy II, M 656, 386.

 27. Siegfried Delius, Vom Fischerdorf zur Hafenstadt, 2nd ed. (Bethel near Bielefeld: Bethel-Mission, 1926), 46. Kwa Kijerumani: “konnte ich den Eindruck mitnehmen, daß Jakobo mit Ernst und Eifer seine Pflicht erfüllte und daß er das Vertrauen der Christen und besonders auch seiner Mitarbeiter in vollem Maße genoß.”

 28. Tazama DACB wasifu wa Paulo Pera (Mprotestanti, Tanganyika) sehemu ya pili ya kipengele cha mwishoni.

 29. Franz Gleiss aliishi na kufanya kazi Milima ya Usambara kuanzia 1894 hadi 1922 (1902/03 likizoni nyumbani), na halafu tena kuanzia 1926 hadi 1939.

 30. Hermann, 10. Kwa Kiingereza: “It was a great day. Thousands of Christians came to Vuga to witness this occasion. It was like a wedding ceremony. Immediately after our ordination we began our ministry by celebrating the Lord’s Supper.”

 31. Kwa mfano: Franz Gleiss, An meinen Hirten (Bethel near Bielefeld: Bethel-Mission, 1926): hasa ukarasa 9-18; lakini pia maandishi mengi katika nyaraka tofauti mbalimbali.

 32. Autobiography II, M 656, 390f.

 33. Franz Gleiß, Die Rückkehr (Bethel near Bielefeld: Bethel-Mission, 1926).

 34. Ernst Damman aliishi na kufanya kazi Tanga kuanzia 1933 hadi 1936.

 35. Yakobo Lumwe, Eine Reise nach Bukoba, übersetzt und bearbeitet von Ernst Dammann, (München: Wilhelm Fink Publishing House, 1996).

 36. Dammann, 3.

 37. Karl Wohlrab aliishi na kufanya kazi Tanga kuanzia 1936 hadi 1939.

 38. Imanuel Ng’anzi Vesso alibatizwa tarehe 2 Desemba 1906, alibarikiwa kuwa mchungaji tarehe 8 Juni 1937, na kufariki tarehe 3 Julai 1961.
 39. Matayo Jengo alibarikiwa kuwa mchungaji tarehe 19 Novemba 1939.

 40. Tarehe zake hasa za kukaa kwake Dar-es-Salaam ni vigumu kuziyamkinisha, lakini yeye mwenyewe aliandika kwenye barua yake ya tarehe 6 Juni 1949 (Wuppertal, M 658, 284f), ya kuwa aliishi Dar-es-Salaam kuanzia 1943 hadi 1947.

 41. S. Hjalmar Swanson, Touring Tanganyika (Rock Island: Augustana Book Concern, 1948), 211.

 42. Hermann, 13.

 43. Dammann, 3f.

 44. Karl Roehl alitafsiri Biblia katika lugha ya Kiswahili na kuchapishwa mwaka wa 1939.

 45. Godfrey P. Hermann, in Hermann, 27.

 46. Mwaka 1959/60 Kanisa la Kiinjili la Usambara Digo lilosambaa ukanda wa pwani kuzunguka mji wa Tanga na kuunganisha na Milima ya Usambara lilipitisha katiba lake ya kwanza na kufanikia huru. Katika mwaka wa 1963 liliundwa pamoja na makanisa mengine sita na kuunda Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanganyika (KKKT).

 47. Makanisa ya Kilutheri ya Tanganyika, Usharika wa Kana - Tanga, Kitabu cha Mazishi (Tanga, 1969ff), No. 42.

 48. Autobiography II, M 656, 393.

Makala haya yalipokelewa katika 2007, na kufanyiwa utafiti na kuandikwa na Mchungaji Dr. Christian Pohl, mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Bavaria (ELCB). Wasifu hawa wa KAWAKIA wako chini ya makala aliyoandika yeye “Tansanische Apostel - Der Lehrer und der Pastor” (Mitume wa Kitanzania - Mwalimu na Mchungaji) katika kitabu Länderheft Tansania, Weltmission heute, Nr. 62 (Tanzania - Missioni ya Ulimwengu Leo No. 62) kuchapishwa na Evangelisches Missionswerk EMW (Umoja wa Makanisa ya Waprotestanti na Sharika za Missioni) katika Hamburg. Katika PhD yake, yaliyotolewa Berlin 2016, kuna maelezo ya undani zaidi juu ya Yakobo Lumwe na watumishi wenyeji wengine wa kanisa la eneo hili: “Die evangelische Mission in Tanga und im Digoland. Der Beitrag einheimischer Mitarbeitender zur Kirchwerdung 1890 - 1925 (Missioni ya Kiprotestanti katika Tanga na Udigo (Tanzania). Watumishi Wenyeji wa Kanisa Walichangia Kuanzishwa kwa Kanisa 1890 - 1925).

Mkalimani: Mchungaji Richard J. Hermas (1941 - 2008), Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tansania, Dayosisi ya Kaskazini Mashariki


Nyumba ya sanaa ya Picha

Yakobo Lumwe