Bure Ukusanyaji wa KAWAKIA

Vifungu vyote viliunda au kuwasilishwa wakati wa miaka ishirini ya kwanza ya mradi huo, kutoka 1995 hadi 2015.

Zebedayo, Yohana Makaranga

1923-2011
Kanisa la Inland la Afrika
Tanzania

Yohana Makaranga Zebedayo alizaliwa mwaka 1923, mwezi wa tatu, tarehe 16 katika kijiji cha Ibaya, Ngudu, wilaya ya Kwimba, mkoa wa Mwanza, Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania.[1] Kabila lake likiwa ni Msukuma na aliishi maisha yake yote Usukumani. Aliitwa Makaranga (jina la ukoo, likiwa na maana ya ‘karanga’) au Ngw’ana Moneki (kwa kisukuma lina maana ya ‘mtoto mzuri’ na aina ya mchezo fulani). Majina haya yalibadirika baada ya kubatizwa Yohana.[2]

Baba yake, Zebedayo Ngaraba Ndonho, au Ngw’ana Sengule, alikuwa mkulima na mwinjilisti katika kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) katika sehemu mbalimbali mpaka kustafu kwake katika Nyashimba, wilaya wa Magu, Mwanza.[3] Anakumbukwa kwa utoaji mzuri kwa kanisa lakini pia kuwa mkari kuhusu waumini wa kanisa lake kutoa moja ya kumi ya mavuno yao. Mkewe alikuwa mpole.[4] Yakobo, mzaliwa wa kwanza wa Zebedayo, alikuwa mchungaji wa AICT na alianzisha kanisa katika kijiji cha Badugu, karibu na Nyashimba. Yohana alikuwa mtoto wa pili kuzaliwa, alifuatwa na Seke na Keferine. Wakati Yohana akiwa mdogo familia ya Zebedayo ilihamia katika kijiji cha Bulima na baadaye kijijini Chumve. Baadaye familia ilianzisha makazi ya kudumu huko Nyashimba.

Ndoa na Elimu

Mnamo mwaka 1946, Yohana alimwoa Elizabeti Nkindikwa Mpanga.[5] Familia ya Elizabeti iliishi karibu na familia ya Zebedayo kijijini Nyashimba na walikuwa marafiki. Ndoa yao ilifanyika katika mila na utamaduni wa kisukuma wa kulipa mahali ulioshuhudiwa na wazee wa pande zote mbili. Kipindi hicho hakukuwa na harusi za kikanisa. Yohana na Elizabeti walizaa watoto sita wakike na wawili wakiume. Wakike walikuwa; Teleza, Helena, Raheli, Agness, Debora na Sara. Wakiume walikuwa; Zebedayo na Lameck.[6] Mpaka kifo cha Yohana yeye na Elizabeti walikuwa na wajukuu 49 na vitukuu 55.[7]

Yohana alisoma katika shule ya misheni ya Africa Inland Mission (AIM) iliyokuwa kijijini Bulima kuanzia mwaka 1950.[8] Walimu wake walikuwa watanzania na walifundisha kwa kisukuma. Ngw’ana Shimba alikuwa mmoja wa walimu wake. Katikati ya masomo yake, lugha ya kufundishia ilibadirika na kuwa Kiswahili.[9] Na alijifunza kiasi lugha ya Kiingereza. Alitembea umbali wa kilometa kumi kutoka Nyashimba kwenda shule kila siku. Alipomaliza masomo alirudi nyumbani na kujishughulisha na ufugaji na kilimo.[10]

Ukristo na Ubatizo

Yohana alilelewa katika familia ya wakristo na haijulikani alianza kumwamini Yesu ni Bwana wakati gani. Alifuata njia tofauti na baba yake katika ujana wake kwa kuvuta sigala, kunywa pombe, na kucheza mcheza ngoma za asili ya kisukuma.[11]  Alimrudia Bwana mnamo mwaka 1946 muda mfupi baadaya kumwoa Elizabeti.[12]  Desturi na matokeo ya ngoma za asili alizocheza zilimtenga na jamii ya kikristo kabisa na hata mkewe na familia yake.  Kwa vile mkewe Elizabeti alikuwa anenda kanisani pamoja na pande zote mbili za wazazi wao, wengi walikuwa wanasema huyu naye awe anamwacha mke wake nyumbani?  Ikawa haieleweki.”[13]  Maana katika mila za kisukuma mwanamke hapaswi kumwachia mji mmewe kwa hiyo ilikuwa aibu kwa Yohana kuachiwa mji na mkewe kwenda kanisani siku ya Jumapili.  Hata Yohana angejaribu kumkataza mkewe asiende baba yake na baba mkwe wake wangemruhusu kwenda kanisani.  Aidha jamii ingemwona Yohana mdhaifu kwa kuachiwa mji na mkewe.[14]  Kwa hiyo shinikizo la jamii, la familia na la marafiki, lilichangia pakubwa katika yeye kubadirika kuwa Mkristo.  Yohana na Elizabeti walisali kanisa la baba yake la AICT Nyashimba kipindi kile.  Silas alidokeza kwamba Yohana alipobadirika alibadirika kweli kweli na akawa Mkristo mzuri, alienda kanisani, na familia yake ikatulia.[15]

Kabla ya ubatizo, Yohana alisoma katekisimu kwa muda wa mwaka mzima.  Baba yake Yohana alifundisha katekisimu kila Jumatano jioni baada ya kipindi cha maombi.  Wanafunzi wa katekisimu walikariri na kurudia kwa sauti waliokariri mafundisho ya msingi ya elimu ya kikristo na jinsi ya kuomba kwa kisukuma.  Walijifunza pia tenzi za rohoni zilizoandikwa kwa kisukuma kilichonunuliwa kutoka duka la vitabu vya kimisionari Bulima na nyimbo za kisukuma zilizotungwa kwenye Biblia.[16]  Baada ya miaka mitatu ya ukristo wake na baada ya kumaliza mafunzo ya katekisimu alibatizwa na mchungaji Yeremiah Mahalu Kisula.[17]

Mwanzo ya Huduma na Mafunzo ya Kikristo

Yohana alianzia uzee wa kanisa katika kanisa la baba yake akiwa na miaka therathini pamoja na Silas Shipula na James Ludoke watu wa rika lake na marafiki zake.  Kupata mzee wa kanisa wazee wa kanisa na mchungaji walipendekeza majina ya wagombea kwanza.  Halafu mchungaji aliyatangaza majina mbele ya waumini ili wapigiwe kura na siku ya kupiga kura.  Baada ya wiki tatu wakristo waliobatizwa walipiga kura kuwachagua wazee wapya.  Yohana, Silas na James walipata mafundisho ya uzee wa kanisa kutoka kwa Amuri, Hezroni Nyanda, Zakayo Rugeye na Jushua Duhu ambao walikuwa wazee wa kanisa lao.[18]

Baada ya miaka kupita kwa maneno ya Silas Shipula ambaye alikuwa mjumbe wa synod kipindi kile, Yohana “alionekana ameamua kumtumikia Bwana.”[19]  Kwa uwezo aliokuwanao Yohana alichaguliwa na mchungaji Batolomeo Ihema na kubaliwa na wazee wa kanisa kuwa mtumishi alifaa kuwa mwinjilisti.  Viongozi wa ngazi ya juu ya kanisa walimpitisha na mwaka 1973 Yohana alienda Busiya Shinyanga kusoma Chuo cha Mafundisho ya Biblia Kolandoto.  Alimaliza miezi mitatu ya mafundisho ya uinjilisti kwa AICT na baadaye akarudi Nyashimba kufuata nyayo za baba yake katika kazi ya uinjilisti.

Huduma ya Uinjilisti

Majukumu ya uinjilisti wa Yohana yalihitaji moyo wa kujitoa sana.  Katika pastoreti ya Bulima, AICT Shigala ilikuwa moja kati ya makanisa tisa.[20]  Mchungaji Batolomeo Ihema alikuwa akisafiri kwa baisikeli kwa kila kanisa kila wiki.  Kanisa la Dutwa lilikuwa zaidi ya kilometa hamsini kutoka nyumbani kwake.  Huduma zake kwa kanisa la Shigala japo lilikuwa karibu na kijiji chake cha Bulima zilikuwa kwa kawaida kila baada ya miezi miwili alipokuja kuleta Ushirika Mtakatifu.  Kwa hiyo Yohana alikuwa akihubiri kila Jumapili na kila Jumatano kwenye kipindi cha maombi.  Mbali na huduma hizi alifundisha madarasa ya katekisimu.  Hii ilikuwa ratiba ya huduma yake kwa kama miaka therathini.  Alikuwa na muda mchache wa kuanzisha au kuhudumia makanisa mengine.

Aidha kwa cheo chake cha kanisa hakikuwa na malipo ya kifedha.  Hata katika mfumo wa mgawanyo wa sadaka wa AICT Yohana hakupewa gawiwo lolote.[21]  Alipokea msaada wa hari kila baada ya muda na baada ya kustafu alikuwa akipewa msaada wa pesa.  Ingawa alijimudu yeye na familia yake kwa njia ya kilimo na ufugaji.[22]

Muda mfupi baada ya kutoka katika mafunzo ya uinjilisti Yohana alikuwa kati ya waamuzi wa kanisa la AICT ambao walikuwa kama ishirini walioamua kuhamisha kanisa kutoka Nyashimba kwenda shule ya msingi Shigala.  Walipogundua kwamba eneo la shule sio sehemu nzuri ya kukutanika Wakristo walianza kutafuta eneo la kujenga kanisa.  Silas ambaye alikuwa kiongozi wa kisiasa pia alipendekeza eneo la kanisa liliopo sasa.  Chaguo la eneo hili halikuwa chaguo la Yohana lakini pole pole alikubali.[23]

Yohana alikuwa mfadhili mkubwa wa ujenzi wa kanisa pamoja na kuongoza utekelezaji wa ujenzi.  Alitoa mabati nyingi ya kuezekea jengo la matofali ya tope.  Mchango huu ulikuwa mkubwa na unakaribia nusu ya gharama zote za ujenzi.  Kitendo hiki cha ukarimu wake ulimvutia tajiri wa ngombe asiye Mkristo (Kalunde Masunga) kijijini mpaka yeye pia akatoa mabati kwa kuezekea kanisa.[24]

Kati ya kazi kubwa katika huduma yake Yohana na timu ya wazee wa kanisa ilikuwa kuwatembelea watu wa kanisa lake mara kwa mara.  Huduma hii ilifanyika hasa kwa watoto.  Wakati wa kilimo viongozi hawa walijituma kuzitembelea familia za watoto wa kikristo.  Hasa waliwaangalia watoto hawa kama wamebadirika, wanawasikiliza wazazi wao, wanafanya kazi za nyumbani, na si kukaa tu.  Jina la “kanisa ya akina [Yohana] Zebedayo na [Silas] Shipula” lilivuma na kukubaliwa kwa sababu hiyo na kanisa likajaa waumini.  Wakati kanisa linahama kutoka shule ya msingi kwenda kwenye jengo jipya lilikuwa na waumini themanini.[25]  Kipindi Yohana anastafu kanisa lilikuwa na waumini mia moja ishirini na watoto wengi.[26]

Sifa na Matokeo yake

Yohana alikuwa na sifa mbalimbali zinazomfanya akumbukwe.  Sifa ya kwanza kubwa ni uimara wa imani yake katika Yesu Kristo na uaminifu katika kazi ya kanisa.  Ikumbukwe kwamba wakati wa Yohana jamii ilipata tiba ya kienyeji ambayo iliambatana na imani za kishirikina lakini Yohana alikataa tiba kutoka kwa waganga wa kienyeji wenye imani za kishirikina.  Imani ya Yohana ilionekana zaidi kipindi cha miaka kumi na moja ya mwisho wa uhai wake alipougua kansa ya kibofu cha mkojo na magonjwa mengine.  Pamoja na kupata upasuaji mwaka 2003 na 2007 lakini afya yake iliendelea kudhofika.[27]  Wakati huu wa ongonjwa wake Ambukile Mwasapile, mponyaji aliyejitokeza huko Loliondo Kaskazini mwa Tanzania akipata umaarufu wa kimataifa mtoto wake Lameck alimshauri na kumtumia hela kutoka Dar es Salaam ili baba yake apate tiba pale.[28]  Yohana alikataa kwa nguvu akisema “kwenda huko ni kwenda kupoteza uhai wangu wa Mungu.”[29] Alikataza familia yake isiende huko kwa matibabu pia.[30]

Imani ya Yohana imeacha alama isiyofutika kwa John Silas ambaye alikuwa mtoto.  John Anakumbuka kipindi cha ukame mbaya Yohana alitangaza kanisani kwamba “Walio na imani kesho mrudi hapa kanisani tutamwomba Mungu mpaka itakaponyesha mvua hatutarudi nyumbani.”  Kesho yake asubuhi John na kaka yake Japhet pamoja na baba yao walirudi kanisani kwa maombi.  Ghafula upepo mkali ulivuma kutoka Kusini na wale waliokuwa wanaomba walianza kushangilia kwamba Mungu amewasikia maombi yao.  Muda wa saa tisa mchana kulikuwa na mvua kubwa sana.  Tukio hili liliendelea kumtia moyo John kuwasaidia watoto katika kukuwa imani yao ya kikristo na imekuwa motisha mkubwa katika uamuzi wake wa kuanzisha na kuendesha shule ya kikristo Shigala.[31]

Sifa ya pili itakayokumbukwa ni kuwa mkweli na uadilifu wake.  Alikuwa msimamizi wa utoaji wa zaka ya mavuno na mbegu zilipohitajika kwa kupanda na muumini akakosa Yohana angempa.[32]  Ukweli na usimamizi mzuri unathamaniwa katika kanisa la Shigala mpaka leo kwa sababu ya mfano wa Yohana.  Kwa mfano siku moja Yohana alisimama kanisani machozi yakimtililika kuomba kujihudhuru kwa sababu ya mtoto wake alipewa mimba nje ya ndoa.  Yohana aliamini kwamba dhambi hii iko ndani ya malango yake na kudhofisha ushuhuda wa uongozi wake.  Baadaya kutiwa moyo na kushauriwa kutoka maandiko matakatifu na wazee wa kanisa Yohana alishawishika kuendelea na kazi hiyo.[33]

Sifa ya tatu ya Yohana ilikuwa ni ukarimu na moyo wa utoaji kwa watu.  Sifa hii ya ukarimu ilikuwa imepandikizwa kwake na mama yake ingawa moyo ya utoaji ilikuwa sifa ya familia ya baba yake.[34]  James Ludoke anakumbuka kwa shukurani Yohana alikuja mara kwa mara na watu kumwombea mkewe aliyekuwa mgonjwa kuanzia siku ya ugonjwa mpaka siku ya kuaga dunia.  Yeyote aliyeenda kwa Yohana alipata msaada.[35]  Silas anakumbuka mfano mwingine wa moyo wake wa utoaji.  Siku moja mvulana aliyeitwa Pharles Masanja alifika nyumbani kwa Silas.  Pharles alitembea kutoka nyumbani kwao Bunda umbali wa kilometa themanini.  Pamoja na wazazi wake kuwa na uwezo wa kumsomesha walikataa kulipa ada ya shule ya sekondari.  Pharles alifaulu kujiunga na masomo ya sekondari lakini wazazi hawakuona sababu ya msingi aendelee na masomo.  Silas alimpeleka Pharles kwenda kumwona Yohana na akamshauri Yohana amsomeshe.  Yohana alikubari kuchukua huo mzigo mkubwa.  Aliuza angalau ng’ombe moja kuhakikisha kwamba Masalu anamaliza masomo yake ya sekondari.[36]  Vile vile Masalu mtoto wa shemeji yake na Yohana alitembea kutoka Bunda mpaka nyumbani kwa Yohana na alisomeshwa kwa masomo ya shule ya sekondari.  Yohana aliwasomesha wengine pia kama Yohana Madundo.[37]

Sifa ya nne ya Yohana ilikuwa anatambua vyema uzuri wa mahubiri na mafundisho ya kibiblia.  Mafundisho yake rahisi na thabiti yalilifanya kanisa la AICT Shigala kukuwa kithiolojia kulinganisha na makanisa mengine katika eneo hilo.  Kwa sababu ya elimu ndogo ya Biblia aliyopata mafundisho yake kuwa hasa juu ya injili ya Yesu Kristo tofauti na wahubiri wengine wa leo wa kiAICT.  Kile alichokijua kutoka Maandiko Matakatifu alikifundisha na kutekeleza kama baba yake kwa uhakika.[38]

Siku za Mwisho za Uhai

Yohana alistafu kazi mwinjilisti mwaka 2002.  Kujihudhuru kwake kuliharakishwa na ugonjwa wa kansa ya kibofu cha mkojo mwaka 2001.[39]  Baada ya kujihudhuru aliendelea kuwa mshauri pale ambapo uongozi wa kanisa ulihitaji msaada.  Hata alipokuwa mgonjwa sana kitandani aliendelea kuwauliza waliomtembelea kuhusu kazi za kanisa.[40]

Yohana Zebedayo alichukuliwa na Bwana tarehe 31 mwezi wa tatu mwaka 2011.  Anakumbukwa kama kiongozi mzuri wa kanisa na kustahili kuigwa kwa mfano wa utauwa wake.  Alikuwa mtumishi mwaminifu wa Kristo mpaka mwisho wa siku zake.  Pia aliwafahamu watu na kuwapenda na alipendwa.[41]

Tafasiri hii imefanywa na Silas John na Abram Kidd


Vidokezo:

 1. Risala ya mazishi, familia ya Yohana Zebedayo, ya Aprili 4, 2011.  Silas Shipula na James Ludoke wanasema alizaliwa Bulima, Nassa.  Silas Shipula na James Ludoke, walihojiwa na mwandishi, Shigala, Magu, Tanzania, Aprili 17, 2012.  Silas na James walikuwa rika moja na marafiki tangu utoto na wafanyakazi wenzake na Yohana Zebedayo katika makanisa ya AICT Nyashimba na Shigala.

 2. Silas Shipula na James Ludoke.

 3. Silas na James wanasema alistafu mwaka 1956.  Silas Shipula na James Ludoke.

 4. John Silas, alihojiwa na mwandishi, Shigala, Magu, Tanzania, Aprili 17, 2012.  John Silas ni mtoto wa Silas Shipula na alimfahamu Yohana Zebedayo kama mwinjilisti wake tangu utoto mpaka kifo cha Yohana.  Alifanya kazi pamoja naye akiwa mzee wa kanisa na mhasibu katika kanisa la AICT Shigala kipindi cha mwisho mwisho mwa uongozi wa  Yohana.

 5. Risala ya mazishi.

 6. Silas Shipula na James Ludoke.

 7. Risala ya mazishi.

 8. Risala ya mazishi inasema kwamba alihudhuria kuanzia 1950 mpaka 1953.  Silas na James wamesema Yohana alikuwa umri kama wa miaka kumi na nane alipomaliza shule ya msingi na kwamba alioa baadaye.  Silas Shipula na James Ludoke.

 9. Silas Shipula na James Ludoke wanasema kwamba badiliko hilo lilitokea mwaka 1952.  Silas Shipula na James Ludoke.

 10. Silas Shipula na James Ludoke.

 11. Ibid.

 12. Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga. Mashihisho ya wasifu ya kwanza, Shigala, Magu, Tanzania, Agusti 14, 2012. Wote ni ndugu zake na Yohana Zebedayo.

 13. Silas Shipula.  Tafasiri ya Mwandishi.

14.  Silas John, mazungumzo na Mwandishi, Bulima, Magu, Tanzania, Agusti 6, 2012.  Silas ni Msukuma Mkristo wa kanisa la Shigala AICT na alimfamahu Yohana pia.

 1. Ibid.

 2. Ibid.

 3. Risala ya mazishi inasema ubatizo wake ulikuwa Agusti 26, 1949, lakini ubatizo wa AIC ulifanyika kipindi cha Pasaka hivyo tarehe hii inamashaka.  Aidha Silas na James wanasema kwamba walibatizwa pamoja na Yohana kipindi cha Pasaka.

 4. Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga. Silas Shipula na James Ludoke walitumia jina Zakayo Kageyo badala ya Zakayo Rugeye.

 5. Silas Shipula, tafasiri ya Mwandishi. Silas Shipula na James Ludoke.

 6. Makanisa mengine katika pastoreti ya Bulima yalikuwa ni; Bulima, Kabita, Mwamanyiri, Chumve, Kalemera, Mkula, Dutwa na Nyangiri.  Silas Shipula na James Ludoke.

 7. John Silas.

 8. Silas Shipula na James Ludoke.

 9. Ibid.

 10. Ibid. Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga. Silas Shipula na James Ludoke wamesema mabati yaliotolewa ilitumiwa kwa nyumba ya Yohana.

25.  Silas Shipula na James Ludoke.

 1. John Silas, mazungumzo kwa njia ya simu na mwandishi, Juni 25, 2012.

 2. Risala ya mazishi.

 3. Cf. Tom Mosoba, “Tanzania: Untold Story of Loliondo Mystery” katika The Citizen (Dar es Salaam) Machi 13, 2011 http://allafrica.com/stories/201103130007.html (ilifunguliwa Juni 26, 2012).

 4. Silas Shipula akimnukuu Yohana Zebedayo.  Tafasiri ya Mwandishi. Silas Shipula na James Ludoke.

 5. Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga.

 6. John Silas akimnukuu Yohana Zebedayo.  Tafasiri ya Mwandishi.  John Silas.

 7. John Silas.

 8. Ibid.

 9. Ibid.

 10. James Ludoke. Silas Shipula na James Ludoke.

 11. Silas Shipula na James Ludoke.

 12. Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga.

 13. Ibid.

 14. Risala ya mazishi.

 15. Silas Shipula na James Ludoke.

 16. Ibid.

Bibliografia:

John Silas, alihojiwa na mwandishi, Shigala, Magu, Tanzania, Aprili 17, 2012.

John Silas, mazungumzo kwa njia ya simu na mwandishi, Juni 25, 2012.

Raheli Yohana, Helena Yohana, Susana Amri, Joyce Luka, Zebedayo Luka, Elizabeti Mpanga (ndugu zake na Yohana), mashihisho ya wasifu ya kwanza, Shigala, Magu, Tanzania, Agusti 10, 2012.

Silas John, alihojiwa na mwandishi, Bulima, Magu, Tanzania, Agusti 6, 2012.

Silas Shipula and James Ludoke, walihojiwa na mwandishi , Shigala, Magu, Tanzania, Aprili 17, 2012.

Tom Mosoba, “Tanzania: Untold Story of Loliondo Mystery” katika The Citizen (Dar es Salaam) March 13, 2011 http://allafrica.com/stories/201103130007.html (ilifunguliwa Juni 26, 2012).

Familia ya Yohana Zebedayo, risala ya mazishi, ya Aprili 4, 2011.


Abram Kidd, mwanafunzi katika masomo ya PhD, AIU, alitafiti na aliandika wasifu hii chini ya uangaliaji ya Babatomiwa Moses Owojaiye alipokuwa AIU.